sualogo

Mtandao wa Ushauri kwa Wakulima

(MUWA)Karibu kwenye maswali ambayo wakulima wanapenda kuuliza.

JINSI YA KULIMA ZAO LA MAHINDI

UTAYARISHAJI WA SHAMBA

1.1 Shamba la mahindi hutayarishwa kulingana na msimu wa kilimo. Kwa kata ya Tindiga ambayo ina vijiji vinne vya MALANGALI, MALUI, KWALUKWAMBE na TINDIGA Utayarishaji wa shamba la MAHINDI unategemeana na msimu wa upandaji, Kwa mahindi ya mwanzo utayarishaji wa shamba huanza mwenzi wa 9 na 10; shughuli zinazofanywa hujumuisha: a) Kulima shamba Shughuli hii mara nyingi hufanyika kwa jembe la trekta b) Kusawazisha ardhi (HARROWING &LEVELLING) Shughuli hii hufanywa kwa kurudia kulima kwa jembe la trekta au kulima kwa jembe la mkono. 1.2 Pia mahindi hupandw amwanzoni mwa mvua za masika yaani mwezi wa pili mwishoni na mwezi wa tatu mwanzoni. Katika msimu huu utayarishaji wa shamba hufanyika mwezi wa pili mwanzoni.


MBEGU ZINAZOTUMIKA

Mbegu bora zilizodhibitishwa zinatumika kwa wingi katika zao hili hasa zile za CHOTARA (hybrid) kama vile SITUKA, Tan 254 n.k.


MUDA WA KUPANDA NA NAFASI ZA UPANDAJI (Time of planting and Spacing)

Kulingana na msimu mahindi hupandwa mwanzonimwa mwezi wa 11 baada ya mvua za kwanza kunyesha (specifically from 1st 15 day of November) ambayo huvunwa mwezi Machi mwishoni au aprili mwanzoni. Pia mahindi hupandwa mwezi Februari mwishoni tarehe 15-28 hadi Machi mwanzoni tarehe 1-6 ambayo huvunwa mwezi Julai katikati na Agosti mwanzoni. Mahindi hupandwa kwa hatua/ nafasi ambazo ni sm80 kati ya mstari na sm 50 kati ya shimo na shimo ambapo mbegu tatu hufukiwa na baadaye miche miwili hubaki kwa kila shimo.


KUPALILIA (Weeding)

Mara nyingi wakulima huandaa mashamba yao VIZURI hivyo kutoa uwezekano wa kuwa na magugu shambani na ikiwa kuna magugu basi palizi ya mkono hufanyika au kwa kutumia viuagugu (HERBCIDES) hasa 2-4D. Palizi hufanywa mara tu magugu yanapoonekana hasa wiki ya pili baada ya mmea kuota.


MATUMIZI YA MBOLEA

Wakulima hutumia mbolea za kukuzia zinazopatikana kwa bei nafuu kama vile BOOSTER (foliage nitrogeneous fertilizers) ambayo hhupigwa kwa kunyunyizia katika majani ya mmea kila baada ya wiki 3, kwa mara 2-3 mpaka mahindi kuvunwa. Kiwango cha kupiga ni mchanganyo wa mls 50-80 ktk lita 15 za maji. Pia wakulima wanatumia mbolea za chumvichumvi wakati wa kupanda na kukuzia. Mbolea zinazotumika kwa wingi ni MINJINGU MAZAO(kg50/ekari = gramu 10kwa shimo wakati wa kupanda) pia mbolea hii huweza kutumika wakati wa kukuzia. Mbolea nyingine ni UREA (KG 50/ekari huwekwa mara mbili shambani yaani kg25 kwa kila muweko mmoja na gramu5 kwa kila shimo ambazo ni sawa na mfuniko wa chupa ya soda)


WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA YANAYOSUMBUA ZAO LA MAHINDI KATIKA KATA NA NJIA ZA KUDHIBITI

A) Viwavi Jeshi Ni wadudu aina ya funza ambao hutokana na Nondo.Hushambulia mahindi kwa kula majaniyake pamoja na shina. Wadudu hawa huangamizwa/kudhibitiwa kwa njia zifuatazo;-

  • Kuondoa vichaka karibu na shamba
  • Kunyunyizia sumu za asili kama vile Mwarobaini majuma mawili ya mwanzo.
  • Kunyunyizia sumu za viwandani endapo wadudu wameanza kuonekana km vile Karate 1ml/1l

B) Funza wa Mabua (Maize Stalk Borer).

  • Funza wa mabua hutoboa shina la mahindi na kusababisha kudumaa kwa mahindi.
  • Matundu, ungaunga kama wa msumeno huonekana kwenye majani yaliyoathiriwa.
  • Mashambulizi huanza juma la pili hadi la tatu baada ya mahindi kuota.

C) Njia za kudhibiti zinazotumika

  • Kuchanganya mahindi na mazao jamii ya mikunde km vile maharagwe
  • Kung oa mahindi yaliyoshambuliwa
  • Sumu za asili mwarobaini
  • Sumu za viwandani km vile Karate


UVUNAJI WA MAHINDI

Mahindi huvunwa mara mbili kutegemeana na wakati wa upandaji, yale yaliyopandwa mwezi wa 11 huvunwa mwezi wa 3 na yale yaliyopandwa mwezi wa 2 huvunwa mwezi wa 7. Baada ya kuvunwa mahindi hukaushwa na kupukuchuliwa na baadaye kuwekwa ktk magunia tayari kwa kuhifadhi au kwa chakula.


UHIFADHI WA MAHINDI

Mahindi huifadhiwa ghalani baada ya kuwekwa viatilifu vya kuzuia bungua wa mahindi Njia za kisasa za uhifadhi hutumiwa kama vile matumiz ya ACTELLIC SUPER DUST katika uwiano wa 1kg kwa gunia 5-10 za ujazo wa 100kg. Kiatilifu kingine ni actellic solution katika rate ya 5mls katika gunia moja la kg 100. Njia nyingine ya kienyeji katika kuhifadhi mahindi ni kuweka juu ya ghala ambalo chini yake kuna jiko la kupikia ambalo hutoa moshi unaotumika kufukuza na kuua wadudu.

UUZAJI WA MAHINDI

Mahindi huuzwa wakati wote katika soko la kila wiki (mnadani) na soko la karibu la wilaya .Kipimo kinachotumiwa ni SADO ambalo ni sawa na kg3-4 na gunia moja linakuwa na sado35Bei ya mahindi inategemea na msimu wakati wa mavuno bei inakuwa kati Tsh1000-1500 kwa sado na wakati usio wa mavuno bei inakuwa kati ya Tsh3000-5000 kwa sado.